Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Mhe. CP Suzan S. Kaganda, amekutana na Waziri wa Masuala ya
Wanawake, Maendeleo ya Jamii, Biashara Ndogo na za Kati wa Zimbabwe, Mhe. Monica Mutsvangwa,
katika Ofisi za Wizara hiyo mjini Harare, kwa lengo la kujadili namna ya kuimarisha ushirikiano
kati ya Tanzania na Zimbabwe katika maeneo mbalimbali ya kimkakati.

Katika kikao hicho, Waziri Mutsvangwa amesisitiza kuwa uhusiano kati ya Tanzania na Zimbabwe
ni wa kindugu na kihistoria, unaotokana na misingi ya harakati za ukombozi wa Kusini mwa Afrika
zilizoasisiwa na waasisi wa mataifa hayo, Hayati Mwalimu Julius K. Nyerere na Hayati Robert G. Mugabe.

Waziri Mutsvangwa ameipongeza Tanzania kwa mchango wake mkubwa katika harakati za ukombozi wa Zimbabwe,
pamoja na juhudi zinazoendelea za kuhifadhi maeneo na nyaraka zinazobeba historia ya ukombozi wa Kusini mwa Afrika.

Aidha, ameipongeza Tanzania kwa juhudi za kuhamasisha matumizi ya nishati safi na kueleza kuwa Zimbabwe
ina nia ya kujifunza na kubadilishana uzoefu na Tanzania kuhusu programu hizo, hususan katika kukabiliana
na ukataji miti na uharibifu wa mazingira.

Kwa upande wake, Balozi Kaganda amesisitiza umuhimu wa kuendeleza na kuimarisha ushirikiano uliopo kati
ya nchi hizo mbili, sambamba na kuanzisha programu za mafunzo, kubadilishana uzoefu na utaalamu, Pamoja
na kusainiwa kwa Hati za Makubaliano (MoU) na mikataba katika maeneo ya kimkakati yenye maslahi ya pamoja.

Aidha, Balozi Kaganda ameipongeza Serikali ya Zimbabwe kwa juhudi zake katika kupambana na ukatili wa kijinsia
(GBV), akieleza kuwa Tanzania pia inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na tatizo hilo.

Ameeleza kuwa Tanzania inatekeleza Mpango wa Pili wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto,
sambamba na kuboresha vituo vya huduma jumuishi na kuimarisha Madawati ya Kijinsia kwa ajili ya kutoa huduma
na ulinzi kwa waathirika wa ukatili.