Tarehe 21 Agusti, 2025, Mhe. Balozi Suzan S. Kaganda akiongozana na timu ya Watumishi wa Ubalozi tulipata fursa
ya kutembelea Mradi wa Geo Pomona Waste Management (PVT) Ltd uliyopo Harare.
Mkurugenzi Mtendaji Dr. Dilesh Nguwaya alitoa ufafanuzi kuwa mradi unajihusisha na
usimamizi na uchakataji wa taka (waste management) ili kuepukana na changamoto ya
uchafuzi wa mazingira katika jiji la Harare.
Ziara hii ni hatua za awali za utekelezaji wa maelekezo ya Waheshimiwa Mawaziri wa
Mazingira wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Zimbabwe
yaliyotolewa pembezoni mwa Mkutano wa COP15 uliofanyika mwezi Julai 2025,
Victoria, Falls Zimbabwe, ambapo ilielekezwa kuwa, timu ya wataalam kutoka Ofisi ya
Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) ya Tanzania ifanye ziara ya kikazi nchini
Zimbabwe kuja kuona na kujifunza ni namna gani Zimbabwe wamefanikiwa kwenye
suala zima la waste management pamoja na biashara ya hewa ya ukaa.
Katika ziara hiyo ujumbe huo ulipata nafasi ya kutembelea maeneo yote yanayohusika na
uchakataji wa taka hizo hadi kufikia hatua ya kuziharibu na nyingine zikitumika kama
chanzo cha kuzalisha nishati ya umeme ambao licha ya kutumika kiwandani hapo, huku
ziada (surplus) ikichangiwa kwenye gridi ya taifa kwa kuuza nishati hiyo kwa shirika la
umeme la Zimbabwe (ZESA).
Mradi huu uliyoanzishwa mwezi Aprili, 2022 katika mpango wa ushirika wa ubia
(Public,Private, Partnership-PPP) unapatikana kwenye eneo lenye ukubwa Kilomita za
Mraba 25,000 la Pomona ambapo awali lilikuwa ni eneo la dampo huku kukiwa na
makazi ya watu. Kampuni hiyo inaendeshwa chini ya mfumo wa PPP imetoa ajira 300
ambapo wengi wao walikuwa ni wakazi wa eneo hilo waliokuwa wakijihusisha na
shughuli ya kuokota taka kwenye dampo ikiwemo chupa za maji na mifuko ya plastic na
kuziuza kwenye taasisi zinazozihitaji.
Ubalozi unaendelea na maandalizi ya ziara ya timu ya wataalam kutoka Ofisi ya Makamu
wa Rais (Muungano na Mazingira) kama ilivyoelekezwa.